"Yule jamaa ni malaya sana" / Dada yule anaonekana ni malaya sana"
Utawasikia watu wakisema maneno hayo kumuashiria mtu fulani. Lakini umeshawahi kujiuliza kuwa malaya ni mtu wa aina gani?
Insha hii tunamchambua mtu huyu "MALAYA" Lakini pia tutaeleza sababu zinazoweza kumfanya mtu kuwa malaya, dalili na athari zake.
___________________________
Mjadala huu utajikita katika kuuzungumzia umalaya kwa kina na tutasimama katika point hizi.
- MAANA YA UMALAYA
- CHANZO / SABABU
- DALILI ZA UMALAYA
- FAIDA ZA UMALAYA
- ATHARI ZAKE
- KUJIKINGA NA UMALAYA
- MATIBABU KWA AMBAYE AMESHAATHIRIKA
- HITIMISHO
1. UMALAYA NINI?
Maana halisi ya umalaya ni;- Kitendo cha mtu kuwa na mahusiano ya kimapenzi au kufanya mapenzi na mtu zaidi ya mmoja kipindi kimoja (Kinyume na sheria maalum kama mila au dini).
Kuwa na mahusiano si jambo geni kwa binadamu, ila kuwa na mahusiano na zaidi ya mtu mmoja na pengine watatu wanne ama na zaidi kwa kipindi kimoja huu ndio umalaya.
Maana hii haihusiani na kitendo cha mtu kuoa kwa ndoa ya kiislamu mke zaidi ya mmoja (Hapana). Ndio maana tukasema kinyume cha sheria ya dini au mila.
2. SABABU / VYANZO VYA UMALAYA
Kila kitu kina sababu zake au chanzo chake. Sababu zinazoweza kumpelekea mtu katika umalaya ni nyingi sana. Lakni hapa tutataja chache tu, nawe unaweza kuongezea chini kabisa ya makala hii sehemu ya Comment.
i) Malezi
'Samaki mkunje angali m bichi'
Malezi ya mzazi / mlezi kwa mtoto yanaweza kumpelekea mwana kutumbukia katika janga hili ovu.
Baadhi ya wazazi wamekuwa wakifanya mambo machafu mbele ya watoto wao bila kujua kuwa mtoto ananakili kile anachokiona kwa mzazi wake na kudhani kuwa ni sawa.
Matusi ya hadharani mbele ya watoto, kuleta michepuko ndani (hasa kwa wazazi wasio na wenza wao) hii ni tabia ambayo inawaathiri sana watoto kisaikolojia.
ii) Utandawazi
Hakuna atakayepinga kuwa utandawazi umekuwa msaada mkubwa sana katika maisha yetu ya sasa. Lakini utandawazi huo huo umekuwa ni changamoto katika vizazi vyetu.
Mitandao ya kijamii imechangia kwa asilimia kubwa kuharibika kwa maadili na watu (hasa vijana) kuingia katika dimbwi hili.
Wazungu na baadhi ya watu wengine walioendelea zaidi katika teknolojia wamekua vipotoshi vikubwa sana kwa vijana wetu kuwaiga tabia zao.
iii) Urithi
'Maji hufuata mkondo'
Hivi unaamini kuwa kuna baadhi ya koo kuwa zina tabia hii? Nadhani utakuwa shahidi wa hili japo kwa kusikia.
Hii ipo katika baadhi ya maeneo ya jamii zetu. Umalaya ni asili tangu kwa mababu na mababu, hivyo mwisho wa siku watoto na wajukuu wanakuwa ni moto wa kuotea mbali.
iv) Makundi
'Ukitaka kuijua tabia ya mtu basi mtazame rafiki yake'
Marafiki waovu wana mchango mkubwa katika kumbadilisha kijana mwema. Nina ushahidi wa hili kwa asilimia zote na nadhani nawe utaniunga mkono.
v) Kuongezeka kwa kipato
'Pesa mwanaharamu'
Kwa baadhi ya watu pesa inakuja na tabia mpya na tabia hizo ikiwemo umalaya. Hii inatuhusu sana wanaume.
Hata akiwa alikuwa na mke basi akizikamata pesa kisawasawa ataanza kutafuta vimada nje na kuanza kuisaliti ndoa yake. Mifano kadhaa imekuwa ni yenye kushuhudiwa maishani mwetu.
vi) Tamaa
'Tamaa mbaya'
Hii zaidi ni kwa dada zetu (sio wote). Kuna muda wanatamani vilivyo zaidi ya uwezo wao na mwisho wa siku kuambukia katika janga la kutumia miili yao kama kitega uchumi (Umalaya).
vii) Changamoto katika mapenzi
Stress za mapenzi hutokana na kusalitiwa, kuachwa, kukimbiwa na mwenza wako zinaweza kukupelekea kuingia katika janga hili kwa aidha kutafuta amani, kumkomesha au kulipa kisasi.
Wengi wanakuja kushituka tayari ameshazama katika lindi hili la uhalifu kutokana na msongo wa mawazo ambao aliupata kwenye ndoa yake au mahusiano.
Changamoto katika mapenzi pia zinaweza kuwa ugomvi ndani ya nyumba au kutokuridhishwa na mwenza wako katika tendo la ndoa.
3. DALILI
Huu ni ugonjwa na una dalili zake kwa ambaye anaanza kuathirika. Ni kama yalivyo magonjwa mengine. Sababu hizi mara nyingi huonekana na wale ambao wapo karibu na mtu husika.
a) Mabadiliko ya tabia
Kubadilika kwa ratiba ya mtu hasa wakati wa kurudi nyumbani, kubadilika kwa marafiki, maneno au mazungumzo kwa mwenza wako.
Mabadiliko yanaweza kujitokeza katika njia nyingi na ambaye atakugundua ni mtu wa karibu yako. Mtu huyo anaweza kuwa mzazi, mlezi, jirani, mpenzi au rafiki ambaye yupo makini na wewe.
b.) Uongo
Huu ni uongo ulokithiri, hasa pale mtu anapoulizwa kuhusiana na mtu ambaye ametiliwa shaka na mwenza wake.
Uongo pia unaweza kuambatana na sababu "a" hapo juu nayo ni pale mtu anatakiwa kueleza juu ya mabadiliko ya tabia yake na kuanza kudanganya (sababu za uongo)
c.) Kutojiamini
Kwa upande wa simu yake inaweza kuwa mgogoro zaidi. Simu inaweza kuwa ina programu nyingi za siri au password / pattern ngumu zaidi na hahitaji mtu mwingine kuifahamu.
Umewahi kusikia mtu anaoga na simu yake? au simu inapoita hutoka na povu bafuni? Basi huyo ni mtu ambaye hajiamini na kutojiamini kwake mara nyingi husababishwa na umalaya.
d.) Kutokuwa na imani na mwenza
Hii kwa ambao wapo katika mahusiano ambayo hayana amani huwa wanajua. Mara nyingi mpenzi ambaye hajatulia huwa anaamini kuwa mwenzake naye pia hufanya hivyo hivyo na kutokumuamini.
Ukiona mwenzi wako hakuamini na huna / hujamuonesha tabia yoyote mbaya basi ujue huenda upande wake kuna shida.
e.) Usiri kupitiliza
Mtu ambaye ameanza tabia ya umalaya huwa hataki mambo yake mengi yajulikane. Hata baadhi ya pesa zake hataki zijulikane na mwenza na wala sio kwa nia nzuri ila ni kwa ajili ya kuweka akiba ya dharura zake na mambo yake machafu.
4. MADHARA YA UMALAYA
- Maradhi
Ukimwi, kisonono, kaswende na magonjwa mengine ya zinaa hayawezi kukuacha kama utajiingiza katika tabia hii. Kibaya zaidi ni kwamba unaweza kumuambukiza ambaye hana hatia kabisa.
- Kifo
Maradhi yanaweza kusababisha kifo lakini pia vifo vya kusababishwa na watu kama kupigwa na kadhalika.
- Ufukara
Kuhonga, kulipia chumba (gest), usafiri na mengine mengi ni miongoni mwa gharama ambazo zinaweza kumpelekea mtu kufilisika kabisa. Mifano iko wazi katika jamii zetu kwa watu ambao waliendekeza umalaya na hatima zao.
Ili kujua zaidi soma makala hii hapa chini nimeelezea kwa kina
- Ulemavu
Kwani inamaana hujawahi kusikia mtu amefumaniwa na kupigwa na hatimaye kujeruhiwa vibaya mpaka kupata ulemavu?
Hii ipo sana katika jamii zetu. Kama hujawahi ona basi ushawahi kusikia walau kwenye vyombo vya habari.
- Kudhalilika
Mtu anakutwa na mke wa mwenyewe na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na mwisho wa siku wanamrusha kwenye mitandao ya kijamii.
Meisho wa siku mtu anaamua kujiua au kuhama mji / mtaa.
- Kukosa amani
Jamaa anatembea na mwanafunzi, ana wasisi juu ya kubeba mimba au laa. Anaona miaka 30 ya jela inamuita.
Kuna mwingine anatafutwa na kuwindwa kama swala porini kwa sababu anatembea na yule mtoto wa mwanajeshi kule mbalizi. Anajua kabisa kuwa akikamatwa huenda ikawa ndio hatima ya maisha / uzima wake.
- Kukithiri kwa watoto wa mitaani
Tumekuwa tukishuhudia mimba zisizo na baba na hali kadhalika watoto wasio na baba ilhali wazazi wao waliwakataa au kukataliwa na wazazi kutokana na tabia hizi kuwa chanzo.
Sambamba na sababu hizi lakini pia baadhi ya madhara ya umalaya ni haya hapa chini.-
- Kukosa amani ndoani
- Kuvunjika kwa ndoa
- Kukosa haiba kwa watu
5. HITIMISHO
Jambo la umalaya limekatazwa karibu na dini zote kubwa duniani. Lakini sambamba na hilo ni jambo ambalo lina hasara nyingi kuliko faida.
Tunakuusia kuepukana na jambo hili ili uweze kuepukana na madhara haya amnbayo yataiathiri jamii yako na afya yako.

Post a Comment